Mpira wa kikapu walia na uhaba wa mashindano

DAR ES SALAAM: KOCHA Mkuu wa timu ya Taifa ya wasichana (U 16) wa mchezo wa kikapu (Basketball), Nelious Mrugeni ameeleza kutokuwa kwa mashindano mengi ya ndani ni sababu kubwa ya kufanya vibaya kwa michezo ya Kimataifa.
Amesema baada ya kutamatika kwa mashindano ya Afrika ya kanda ya tano wachezaji wanarudi mashuleni na wengine katika vituo vyao na kusubiri hadi mwakani katika mashindano hayo.
Julai 15, 2024 kulikuwa na fainali ya mashindano ya U 16 ya Kanda ya tano ya Afrika, Tanzania wasichana ni mabingwa kwa kushinda alama 71 kwa 69 mbele ya Kenya kwa Wanavula Burundi walitwaa ubingwa huo wa alama 65 kwa 53 dhidi ya Tanzania ambaye ni mwenyeji.
Akizungumza na Spotileo, Nelious amesema wanashindwa kufanya vizuri wanapokwenda kwenye mashindano ya kimataifa kwa sababu wanakosa uzoefu wa kucheza mechi nyingi za ndani.
“Tumekuwa na wachezaji wenye vipaji lakini tunakwamishwa na kutokuwepo kwa mashindano mengi, yatakayowapa uzoefu na kufanya vizuri katika michuano mingi, tunapokwenda nje ya Tanzania inatusaidia na kuweza kuleta ushindani,” amesema kocha huyo.
Ameongeza kuwa kushindwa kufanya vizuri wanapokwenda ugenini au ndani katika mashindano ya kimataifa kutokana na kutokuwepo na misingi kuanzia chini na kuwapa nafasi ya vijana kucheza mashindano mengi ya kumjenga na kumpoa ukomavu ambao utamsaidia katika mashindano.