Motsepe asema Afrika imesimama na Infantino

RAIS wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Patrice Motsepe, amesema Afrika itaendelea kumuunga mkono rais wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), Gianni Infantino, katika jitihada zake za kuchaguliwa tena kuongoza chombo hicho katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Machi 18, 2027, mjini Rabat, Morocco.
Motsepe alitoa kauli hiyo Alhamisi wakati wa mkutano wa mkakati wa CAF uliofanyika nchini Cape Verde, akisisitiza kuwa mataifa wanachama wa shirikisho hilo yamekubaliana kwa kauli moja kumuunga mkono Infantino.
“Tulipitisha azimio kwa kauli moja kwamba tunamuunga mkono na tutaendelea kusimama naye katika uchaguzi ujao,” alisema Motsepe.
Baada ya kutoa kauli hiyo, Motsepe aliwataka wajumbe kutoka mashirikisho 54 ya soka ya kitaifa barani Afrika kusimama na kumpigia makofi Infantino, ambaye awali alikuwa ametoa hotuba katika mkutano huo.
Ingawa wajumbe walichukua muda kabla ya kusimama, hatimaye Infantino alipokea makofi ya muda mrefu huku waliohudhuria wakionyesha kumuunga mkono.
Mbali na suala la uchaguzi wa FIFA, Motsepe amesema anaamini kuwa nchi ya Afrika inaweza kutwaa Kombe la Dunia, lakini amesisitiza kuwa mafanikio hayo yanahitaji uwekezaji mkubwa zaidi katika akademi za soka na maendeleo ya wachezaji vijana.
“Moja ya mataifa ya Afrika yatashinda Kombe la Dunia. Lakini tunapaswa kuongeza uwekezaji katika akademi zetu na kwa vijana,” alisema.
Aliongeza kuwa ushirikiano kati ya CAF na FIFA chini ya uongozi wa Infantino ni muhimu katika kuendeleza soka la Afrika.
Motsepe amesisitiza kuwa bara hilo haliwezi kutegemea mipango na ahadi pekee bila kuweka fedha katika utekelezaji wake.
“Hatuwezi kuendelea kuzungumza vizuri tu na kuwa na mipango mizuri. Tunapaswa kuwekeza,” alisema.




