
Kocha Msaidizi wa Yanga, Cedric Kaze amesema mchezo wa Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara dhidi ya Singida Big Stars utakaopigwa Dar es Salaam Novemba 17 utakuwa mgumu.
Kaze amesema hayo leo Dar es Salaam katika mkutano na Waandishi wa Habari kuelekea mchezo huo kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa.
“Mchezo wetu na Singida BS FC ni mchezo mgumu kutokana na ukubwa wa Kikosi cha Singida hasa ukizingatia mwalimu waliye nae (Hans) ni mzoefu sana na amewahi kuitumikia Yanga SC kwa mafanikio” amesema Kaze.
Amesema Yanga ni timu kubwa na inawaheshimu wapinzani wake lakini anaamini timu nyingi zinaihofia klabu hiyo yenya makao makuu Jangwani, Dar es Salaam.
“Haijalishi tunacheza wakati gani na eneo gani lakini najua timu nyingi zinacheza kwa tahadhari kubwa kwa sababu wanajua ubora wetu,” amesema.
Aidha amesema Yanga katika mchezo huo wa Novemba 17 itawakosa baadhi ya wachezaji ambao wamejiunga timu zao za taifa kama Djigui Diarra, Aziz Ki na Gael Bigirimana.