Masumbwi

Mandonga asema huu ni mwanzo

ZANZIBAR. BONDIA Karim Mandonga ‘Mtu Kazi’ ameibuka mshindi kwa pointi dhidi ya Mmarekani Michael Williams katika pambano la ngumi lililofanyika Zanzibar, huku akituma ujumbe mzito kwa mabondia wa kigeni anaotarajia kukutana nao baadaye.

Baada ya ushindi huo, Mandonga amesema pambano hilo lilikuwa mwanzo tu wa safari yake, akisisitiza kuwa bado ana uwezo wa kukabiliana na wapinzani wengine wakubwa zaidi.

“Hili ni mwanzo tu. Nikimpata Mzungu mwingine namtoa roho. Mzungu kaficha jina lake, ubatizo wake, lakini amekanyaga kwa Mandonga, mtu kazi. Wewe hutaki nitakupiga, utake, nitakupiga,” amesema.

Ushindi huo umemfanya Mandonga kuendelea kujenga rekodi yake katika mchezo wa ngumi, huku akionesha nia ya kuendelea kukutana na mabondia kutoka nje ya Tanzania.

Kwa upande wake, Williams amesema hakufanya vizuri katika pambano hilo, ingawa anaamini angeweza kupata ushindi kama pambano lingeendelea hadi raundi zote sita zilizopangwa.

“Lilikuwa pambano zuri. Sidhani kama nilifanya vizuri. Nafikiri nilikuwa nikimpiga vizuri kwa jabs. Alikuwa na makonde machache mazuri, lakini kama pambano lingeenda raundi zote sita kama lilivyopangwa, nafikiri ningeshinda,” amesema Williams.

Williams amesema pambano hilo lilikuwa la kwanza kwake, hivyo amepata uzoefu ambao utamsaidia katika mapambano yake yajayo.

Related Articles

Back to top button