AFCON

Makonda aonya klabu zinazoua vipaji vya wachezaji

RABAT:WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, amevionya baadhi ya klabu vinavyopenda kuwasajili wachezaji wenye umri mdogo kisha kuwaweka benchi kwa muda mrefu bila kuwapa nafasi ya kucheza, akisema tabia hiyo huua vipaji vyao na kuathiri maendeleo ya soka la Tanzania.

Makonda amesema hatua ya kuwasajili wachezaji vijana bila kuwapa muda wa kucheza husababisha maendeleo yao kusimama na wakati mwingine vipaji vyao kufa kabisa, huku majina yao yakibaki kuwa historia badala ya kuwa nyota wa baadaye wa taifa.

Akizungumzia jijini Rabat, Morocco baada ya kumalizika kwa michuano ya Afrika kwa vijana chini ya miaka 17, Waziri huyo amesisitiza kuwa klabu zinazotaka kuwasajili zisifanye hivyo kwa lengo la kuwahifadhi benchi, bali viwahakikishie nafasi ya kucheza ili waendelee kukua na kuimarika.

Katika fainali iliyochezwa jana Serengeti Boys ilishindwa kubeba kombe baada ya kupoteza kwa mikwaju ya penalty 4-2 dhidi ya Senegal kufuatia sare ya bao 1-1 ndani ya dakika 90 na kushika nafasi ya pili.

“Kwa masilahi ya nchi, vijana hawa wanahitaji kucheza ili waendelee kukua na kuimarika zaidi na baadaye walitumikie taifa. Kama mnawasajili kwa kushinda halafu mnaishia kuwaweka benchi, itawasaidia nini?” amehoji.

Makonda amesema mafanikio ya muda mrefu ya soka la Tanzania yanategemea namna ambavyo vipaji vya vijana vitalelewa na kuendelezwa, hivyo ni muhimu kwa klabu kutoa nafasi kwa wachezaji hao kuonesha uwezo wao uwanjani.

Aidha, amemuelekeza Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) pamoja na Oscar Mirambo kutafuta utaratibu utakaohakikisha klabu zitajazowasajili vijana hao zinawapa nafasi ya kucheza na kuendelea kukuza viwango vyao.

Amesema hatua hiyo itasaidia kulinda na kuendeleza vipaji vya wachezaji vijana, kuongeza ushindani wa soka nchini na kujenga msingi imara wa timu za taifa za baadaye.

Related Articles

Back to top button