Masumbwi

Mafia boxing yafungua milango kwa mabondia

DAR ES SALAAM:PROMOTA wa ngumi za kulipwa, Ally Zayumba, amesema fursa zipo wazi kwa mabondia kutoka mikoa mbalimbali nchini wanaotaka kusimamiwa chini ya Mafia Boxing, akibainisha kuwa kipaumbele kikubwa ni nidhamu, mapenzi ya dhati kwa mchezo wa ngumi na kujitoa kikamilifu.

Katika mazungumzo na SpotiLeo Zayumba amesema Mafia Boxing imejipanga kuibua vipaji vipya na kuvilea kwa lengo la kuwasaidia mabondia kutimiza ndoto zao za kufanikiwa katika ngumi za kulipwa ndani na nje ya nchi.

“Tunapokea mabondia kutoka mikoa tofauti ilimradi awe anapenda mchezo wenyewe, awe na nidhamu na awe anajua jukumu lake. Lengo letu ni kuibua vipaji na kuvisaidia kutimiza ndoto zao,” alisema Zayumba,”amesema.

Aliongeza kuwa tayari Mafia Boxing inasimamia jumla ya mabondia 24, tangu walipoanza kupokea mabondia kwa kipindi kirefu, huku idadi hiyo ikitarajiwa kuongezeka kadri mahitaji yanavyoongezeka.

Katika kuongeza ubora na uzoefu wa mabondia wao, Zayumba alisema wamekuwa wakipata programu za nje ya nchi zinazowawezesha kuwapeleka mabondia kufanya mazoezi katika mataifa yaliyoendelea kimichezo ili kujifunza mbinu za kisasa za ngumi.

Aidha, Mafia Boxing imefungua milango kwa mabondia wa kigeni kufanya kazi nao, ambapo hadi sasa tayari wanaye bondia mmoja kutoka Afrika Kusini, hatua inayoongeza ushindani na kubadilishana uzoefu.

Akizungumzia mipango ya mwaka huu, Zayumba alisema Mafia Boxing inatarajia kuandaa mapambano mengi ya rekodi ya mkanda wa WBO, yakitarajiwa kuanza mwezi Aprili, akiwataka mashabiki wa ngumi kujiandaa kwa msimu wenye ushindani mkubwa.

Related Articles

Back to top button