Loemba: Kila mchezo kwetu ni fainali

MCHEZAJI wa Simba SC, Ino Loemba, amesema kwao kila mchezo ni kama fainali jambo linalowafanya wasimdharau mpinzani yeyote wanayekutana naye.
Loemba aliyasema hayo baada ya Simba kutinga hatua ya 16 bora ya michuano ya Kombe la Shirikisho la CRDB kufuatia kuifunga timu ya Championship B19 mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Jenerali Isamuhyo juzi. Mchezaji huyo alifunga bao moja lingine likifungwa na Cleatus Chama.
Alisema kuwa wachezaji wote wana dhamira ya kupambana kwa nguvu katika kila mechi wanayocheza.
“Kila mchezo kwetu ni muhimu kama fainali. Tunakuwa na mtazamo na dhamira ile ile ya kupambana. Hatuchagui mpinzani, iwe Singida, Pamba Jiji au timu ndogo, hatudharau yeyote, tunatoa uwezo wetu wote,” alisema Loemba.
Aliongeza kuwa malengo ya Simba ni kuendelea kupata ushindi katika mechi zijazo ili kufikia malengo ya timu ya kutwaa mataji msimu huu.
Kiungo huyo pia aliwashukuru mashabiki wa Simba kwa kuendelea kuisapoti timu yao, akisema uwepo wao uwanjani unawapa nguvu wachezaji kupambana zaidi.
“Tunafurahi kuwa na mashabiki wetu na tutaendelea kupambana katika kila mchezo ili kupata matokeo mazuri.”




