Kigunduzi cha gesi kutumika Debi ya Kariakoo

DAR ES SALAAM: MTENDAJI Mkuu wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania, Cornel Barnabas, amesema kifaa maalum cha kugundua gesi ‘Gas Detector’ kitatumika katika maandalizi ya Debi ya Kariakoo kati ya Simba na Yanga, kwa ajili ya kufuatilia hali ya hewa na kubaini uwepo wa harufu hatarishi uwanjani.
Hatua hiyo imekuja baada ya kuibuka malalamiko ya mara kwa mara hasa kwa watani hao kuwa vyumba vya kubadilishia nguo hupulizwa dawa na harufu nyingine hatarishi ndio maana wakati mwingine hawaingii au kupita sehemu sahihi.
Mchezo wa Simba na Yanga unatarajiwa kuchezwa Oktoba 10, mwaka huu Dar es Salaam.
Akizungumza Dar es Salaam Barnabas amesema hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za Bodi ya Ligi kuhakikisha mazingira ya uwanja yanakuwa salama kwa wachezaji, mashabiki na wadau watakaohudhuria mchezo huo unaotarajiwa kuvuta umati mkubwa.
Amesema kifaa hicho kina uwezo wa kupima hali ya hewa ndani ya maeneo mbalimbali, ikiwemo vyumba vya kubadilishia nguo, na kutoa taarifa kuhusu kiwango cha oksijeni pamoja na uwepo wa gesi nyingine.
“Tumekuwa na malalamiko mbalimbali kuhusu vyumba vya kubadilishia nguo, wengine wanaingia na kukuta kuna harufu na wakati mwingine wamefikia hatua ya kubadilishia nje ya uwanja. Tunaona hili ni changamoto na lazima tushirikiane na wenye timu na viwanja kuhakikisha tunatatua changamoto hiyo,” amesema.
Barnabas amesema kiwango cha kawaida cha oksijeni katika chumba kinapaswa kuwa asilimia 20.9, hivyo kifaa hicho kitasaidia kubaini iwapo kiwango hicho kipo chini au juu na kutoa vipimo vinavyoweza kusaidia kuchukua hatua stahiki.
Amesema matumizi ya kifaa hicho ni sehemu ya maandalizi mapana ya kuhakikisha Debi ya Kariakoo inafanyika katika mazingira salama kwa wote watakaokuwa uwanjani.




