Mastaa

Khadija Kopa:Diamond ana upendo na mkarimu

DAR ES SALAAM;MALKIA wa Taarabu, Khadija Kopa, amemzungumzia mkwewe, msanii wa Bongo Fleva, Naseeb Abdul ‘Diamond Platnumz’, akimtaja kuwa ni mtu mwenye roho nzuri, moyo wa kusaidia watu na upendo kwa wengine.

Akizungumza kuhusu Diamond, Khadija Kopa amesema kuwa msanii huyo amekuwa akionyesha ukarimu wake kwa vitendo, ikiwemo kumpatia zawadi mbalimbali pale anapoamua kufanya hivyo.

Kopa amesisitiza kuwa ukarimu wa Diamond hauishii kwa watu wa familia pekee, bali pia kwa watu wengine wenye uhitaji.

“Si kwake tu, bali hata nyakati nyingine Diamond anaweza kumsaidia mtu wa nje akipata taarifa kuwa mtu fulani anaumwa na anahitaji msaada wa kitu hiki au kile ili aweze kuwa sawa,” amesema Khadija Kopa.

Aidha, Malkia huyo wa Taarabu ameeleza kuwa Diamond ni mtu anayependa kusikiliza wengine, mkarimu na mwenye uwezo wa kupokea msamaha pale watu wanapotambua makosa yao na kuomba radhi.

Kuhusu mapungufu yake, Khadija Kopa amesema kuwa hakuna binadamu aliyekamilika, kwani kila mtu ana mapungufu yake. Hata hivyo, amemtaja Diamond kuwa ni mwanaume wa nguvu na kumshauri mwanaye, Zuchu, kuthamini na kushikilia kile ambacho Mungu amemjalia.

Kauli hiyo imekuja wakati ambapo uhusiano wa Zuchu na Diamond Platnumz ukiendelea kuzungumziwa na mashabiki wao, huku taarifa zilizotolewa kwenye habari hii zikieleza kuwa wawili hao wana mtoto mmoja.

Related Articles

Back to top button