Khadija Kopa awajibu wanaoibeza gari ya Zuchu

DAR ES SALAAM:MWIMBAJI mkongwe wa muziki wa Taarab, Khadija Kopa, amewajibu watu wanaobeza gari la mwanaye, mwanamuziki wa Bongo Fleva, Zuhura Othuman ‘Zuchu’, kufuatia baadhi ya watu kutoa maoni ya kejeli kuhusu thamani ya gari hilo.
Khadija Kopa ametoa kauli hiyo kupitia ukurasa wake wa Instagram, akionekana kutofurahishwa na namna baadhi ya watu wanavyopokea mafanikio ya mwanaye kwa kuyabeza badala ya kumpongeza.
Katika ujumbe wake aliandika: “Imewauma eeeeeee, hata bado Mungu atawaonesha zaidi.”
Kauli hiyo imekuja kufuatia mjadala ulioibuka mitandaoni kuhusu gari la Zuchu, ambapo baadhi ya watumiaji wa mitandao ya kijamii wamekuwa wakitoa maoni mbalimbali, yakiwamo ya kejeli kuhusu bei na thamani ya gari hilo.
Hata hivyo, ujumbe wa Khadija unaashiria msimamo wake wa kutetea mafanikio ya mwanaye, huku akionyesha kuwa anaamini bado Zuchu ana safari ndefu ya mafanikio na mambo makubwa zaidi yanamngoja.




