Kesi mpya sita kuhusu P. Diddy zaibuliwa

NEWYORK: KAMPUNI ya Sheria ya Buzbee imeeleza mpango wake wa kuwasilisha mashtaka ya ziada dhidi ya mwanamuziki na mfanyabiashara Sean Combs maarufu P. Diddy kwa unyanyasaji wa kijinsia katika wiki zijazo.
Jumatatu P. Diddy alifunguliwa mashitaka mapya sita ya unyanyasaji wa kijinsia. Diddy anakabiliwa na kesi sita mpya za unyanyasaji wa kijinsia zilizofikishwa Jumatatu, ikiwa ni pamoja na kumshutumu msanii huyo kumpiga mtoto mdogo.
Kesi zote hizo zitasikilizwa mwakani 2025. Wakili Tony Buzbee mwenye makao yake Houston, ndiye aliyewasilisha mashtaka hayo akidai kwamba anawakilisha watu 120 wanaomtuhumu Combs kwa unyanyasaji.
Hata hivyo Combs amekanusha kutenda makosa yote katika kesi nyingine za madai dhidi yake.
Kesi hizo ziliwasilishwa katika mahakama ya shirikisho ya New York na walalamikaji wasiojulikana, akiwemo mtu mmoja ambaye anamtuhumu Combs kwa kumshambulia alipokuwa mtoto.
Mlalamikaji alidai kuwa wakati wa tafrija kwenye jumba la Combs’s Hamptons mnamo 1998, rapa huyo alimwelekeza kuvua suruali yake kisha akamshikashika sehemu zake za siri. Alisema wakati huo alikuwa na umri wa miaka 16.
“Kwa miongo kadhaa, Sean Combs aliwanyanyasa, kuwabaka, kuwashambulia, kuwatishia na kuwalazimisha wanawake, wanaume na watoto wadogo kwa ajili ya kujiridhisha kingono, kudai kutawala na kuficha tabia yake ya kuchukiza,” ilisema moja ya mashtaka yaliyowasilishwa na mlalamikaji John Doe.
“Ukweli utashinda: Combs hajawahi kumdhulumu mtu yeyote kingono – mtu mzima au mdogo, mwanamume au mwanamke,” mawakili wa Combs walisema katika taarifa Jumatatu.
Combs alikamatwa mnamo Septemba na kushtakiwa kwa makosa matatu ya uhalifu wa kula njama, biashara ya ngono na usafirishaji ili kujihusisha na ukahaba. Alikanusha hatia mnamo Septemba 17.
Hakimu alikataa ombi la Combs la kuachiliwa kwa dhamana mnamo Oktoba 10 na akapanga tarehe ya kusikilizwa kwa kesi Mei 5, 2025.