Ligi Kuu

Imevuja! Yanga yashusha kifaa

KATIKA kuimarisha kikosi cha Yanga, uongozi wa klabu hiyo umeweka wazi kwamba umeshusha kifaa kipya kutoka nje kwa ajili ya dirisha dogo la usajili.

Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe ameliambia gazeti hili kuwa hivi karibuni Rais wa klabu hiyo, Hersi Said aliweka wazi kuwa atashusha nyota wapya wawili katika dirisha dogo la usajili litakapofunguliwa baadaye mwaka huu.

Licha ya Kamwe kutoweka wazi jina na nafasi ya nyota huyo, Spotileo leo limeelezwa kuwa Yanga wamemleta kiungo Charve Onoya kutoka klabu ya As Maniema ya DR Congo.

Kiungo huyo alitakiwa kujiunga na Yanga mwanzoni mwa msimu huu, lakini dili lilifeli na safari hii mabosi wa klabu hiyo wamerejea kwa nguvu zote kumleta nyota huyo ambaye inadaiwa yupo hapa nchini.

Amesema miongoni mwa nyota hao wawili, mmoja ametua nchini Jumamosi Oktoba 19, akiambatana na kipa wao, Djigui Diarra ambaye alikuwa kwenye majukumu ya timu ya Taifa.

“Huyo mchezaji aliyemsema Rais Hersi tumemleta alikuwepo uwanjani katika mchezo wa Dabi ya Kariakoo na amekuja kufanya mazungumzo na kusajili tayari kwa kuanza kazi katika michuano ya kimataifa,” amesema Kamwe ambaye hakutaja jina wala nafasi anayocheza mchezaji huyo.

Amesema licha ya kikosi cha Yanga kuonekana ni ’tishio’, lakini  wanaona hakijakamilika katika kiwango wanachohitaji, bado wanataka kuona Yanga iliyokuwa bora na imara.

“Nataka niwaambie tu, Yanga hii bado, Januari kutakuwa na ongezeko la mchezaji mwingine wa kigeni. Kwa hiyo haijakamilika, tunahitaji kuchukuwa ubingwa wa Afrika,” amesema Kamwe.

Related Articles

Back to top button