Hayawi hayawi, yamekuwa
ENGLAND: Baada ya kusubiriwa muda mrefu hatimaye kesi maarufu ya Ligi kuu ya England inayowakabili mabingwa mara 4 mfululizo wa ligi hiyo Manchester city kuhusu mashtaka 115 dhidi yao ya uvunjifu wa sheria za matumizi ya fedha za usajili wa wachezaji itaanza Jumatatu ijayo ya Septemba 16.
Kwa mujibu wa Sky Sports News vigogo hao wa soka la England watasimama mbele ya Pilato kusikiliza shauri hilo ambalo bodi ya ligi kuu ya England iliifungua dhidi yao
Manchester City wameshtakiwa kwa kuvunja sheria hizo kwa kipindi cha miaka tisa, kilichoanza 2009 hadi 2018. Katika kipindi hicho, Man City ambao tayari wamekana mashtaka yote dhidi yao, walitwaa ubingwa wa Ligi hiyo mara tatu.
Klabu hiyo inatuhumiwa kwa makosa mbalimbali ikiwemo kushindwa kutoa taarifa sahihi za kifedha, kufunja kanuni za faida na mapato za ligi hiyo, kushindwa kufuata kanuni za usawa katika matumizi ya fedha za UEFA
Ikiwa itakutwa na hatia, Manchester City itakumbana na adhabu mbalimbali ikiwemo kukatwa pointi, faini kubwa, kufungiwa usajili na hata kufungiwa kushiriki michuano inayoandaliwa na UEFA