Doku arejea Ubelgiji, Lukaku nje

UBELGIJI: KOCHA wa timu ya taifa ya Ubelgiji, Mark van Bommel, amepata nguvu mpya baada ya winga Jeremy Doku kurejea kikosini kufuatia kupona jeraha lililomuweka nje ya michezo minne ya mwanzo ya kampeni ya Ligi ya Mataifa Ulaya (UEFA Nations League), huku mshambuliaji Romelu Lukaku akikosekana kutokana na maumivu ya nyonga.
Doku, ambaye alikosa michezo ya Septemba na Oktoba kutokana na jeraha, sasa yuko fiti kwa ajili ya mechi mbili za mwisho za Kundi A1 dhidi ya Uturuki mjini Izmir Alhamisi na Italia mjini Brussels Jumapili.
Van Bommel alisema amefurahishwa na kurejea kwa Doku, akieleza kuwa uwepo wake unaongeza ushindani katika nafasi za winga, ingawa unampa changamoto ya kuchagua kikosi cha kwanza kutokana na kuwa na wachezaji watano wenye uwezo wa kucheza pande zote mbili za uwanja.
Hata hivyo, Ubelgiji italazimika kucheza bila Lukaku, ambaye ni mfungaji bora wa muda wote wa timu hiyo. Kocha huyo alisema mshambuliaji huyo alianza kusumbuliwa na maumivu ya nyonga na baada ya makubaliano wameamua kutomhusisha katika mchezo ujao ili kuepusha hali yake kuwa mbaya zaidi.
Van Bommel alieleza kuwa Lukaku ni mchezaji muhimu ndani na nje ya uwanja, licha ya kuanza mchezo mmoja pekee hadi sasa, huku akitumaini mshambuliaji huyo atakuwa fiti kabla ya pambano dhidi ya Italia.
Ubelgiji kwa sasa inashika nafasi ya tatu katika Kundi A1 ikiwa na pointi sita, nyuma ya vinara Ufaransa wenye pointi 10 na Italia yenye saba. Timu mbili za juu ndizo zitakazofuzu kwa robo fainali zitakazochezwa Machi mwaka 2027. Ufaransa itakutana na Italia mjini Milan Alhamisi katika mchezo mwingine muhimu wa kundi hilo.



