Mombasa Rugby yapata udhamini wa milioni 92 kurejesha Kenya CUP

MOMBASA: KLABU ya Mombasa Sports Club Rugby imepata udhamini wa Shilingi za Kenya milioni 4.5 sawa na takribani Shilingi milioni 92 za Tanzania katika jitihada za kuimarisha kikosi chake na kurejea katika mashindano ya Ligi Kuu ya Raga ya Kenya (Kenya Cup).
Fedha hizo zitatolewa na kampuni ya usafirishaji wa mizigo ya Mitchell Cotts Freight Kenya Limited kupitia mkataba wa miaka mitatu unaoanzia msimu wa 2026/27 hadi 2028/29.
Chini ya makubaliano hayo, klabu hiyo itakuwa ikipokea Shilingi milioni 1.5 kila mwaka kwa ajili ya kugharamia shughuli mbalimbali za timu.
Msaada huo unatarajiwa kusaidia kugharamia usafiri, malazi, chakula, vifaa vya michezo pamoja na maandalizi na uendeshaji wa mechi.
Mitchell Cotts Freight Kenya Limited si mara ya kwanza kushirikiana na klabu hiyo, kwani iliwahi kuwa mdhamini wa jezi zake katika msimu wa 2025/26.
Akizungumzia udhamini huo, mwenyekiti wa Mombasa Rugby, Rogers Otieno Lai, amesema fedha hizo zitaimarisha shughuli za klabu na kuongeza uwezo wake wa kupambana kurejea katika mashindano ya daraja la juu nchini Kenya.
Mombasa Rugby inatarajiwa kuanza kampeni yake ya michuano ya Kenya Rugby Championship kwa kucheza ugenini dhidi ya South Coast Pirates, Novemba 21, 2026.
Msimu huo utakuwa na jumla ya mechi 11 na unatarajiwa kukamilika Machi 13, 2027, huku michezo mitano ikipangwa kuchezwa katika uwanja wa Mombasa Sports Club.
Mbali na timu ya wakubwa, makubaliano hayo pia yataisaidia klabu kuimarisha programu za raga kwa vijana na jamii, zinazolenga kukuza vipaji vya wachezaji chipukizi katika eneo la Pwani.
Programu hizo zinatoa fursa kwa vijana kuendeleza vipaji vyao na kupata nafasi ya kujiunga na kikosi cha wakubwa.
Kwa sasa, jukumu kubwa la Mombasa Rugby ni kutumia vyema uwekezaji huo kuimarisha maandalizi, kufanya vizuri uwanjani na kupambana kupata nafasi ya kupanda daraja na kurejea Kenya Cup.




