CRDB Foundation kutunuku zaidi ya Milioni 100 kwenye Imbeju ndondo Cup 2026

DAR ES SALAAM:BENKI ya CRDB kupitia CRDB Foundation imeahidi kutoa zawadi zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 100 katika mashindano ya Imbeju Ndondo Cup 2026, yatakayokuwa msimu wa 13 tangu kuanzishwa kwa mashindano hayo.
Kwa mujibu wa mwaandaaji, Shafii Dauda amesema bingwa wa mashindano hayo atajinyakulia sh. milioni 30, huku mshindi wa pili akipata sh.milioni 15. Mbali na zawadi hizo, kutakuwa na zawadi mbalimbali zitakazotolewa kwa washiriki na wadau wa mashindano, ikiwemo sh.100,000 (laki 1)kwa mchezaji bora na shabiki bora katika kila mechi.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mashindano hayo jijini Dar es Salaam, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule, ameipongeza Benki ya CRDB kwa kuendelea kuunga mkono bunifu na vipaji vya vijana nchini kupitia michezo na programu mbalimbali za maendeleo.
Naye Mkurugenzi wa CRDB Foundation, Tully Esther Mwambapa, amesema lengo la taasisi hiyo si kuendeleza vipaji vya michezo pekee, bali pia kuwajengea vijana maarifa, maono na fursa za kuboresha maisha yao.

“Tunataka kuona kila kijana anayeshiriki Imbeju Ndondo Cup anatoka hapa akiwa si mchezaji tu, bali pia akiwa na maarifa zaidi, maono makubwa na fursa za kufanikiwa kimaisha,” amesema Mwambapa.
Mashindano ya Imbeju Ndondo Cup yameendelea kuwa jukwaa muhimu la kuibua na kukuza vipaji vya soka kwa vijana, huku yakitoa mchango mkubwa katika maendeleo ya michezo na ajira kwa vijana nchini.




