Clara Luvanga atupia, aweka rekodi Marekani

TEXAS: MSHAMBULIAJI mpya wa Washington Spirit, Clara Luvanga ameanza kuonesha makali yake baada ya usiku wa kuamkia leo Jumatatu kufunga bao na kuipa ushindi timu hiyo dhidi ya Houston Dash.
Washington iliibuka na ushindi wa mabao 3-2 ikiwa ugenini Uwanja wa Shell Ernegy, Houston na Clara alikandamiza bao la tatu dakika ya 84.
Kwa bao hilo, Clara ameweka rekodi ya kuwa Mtanzania wa kwanza kufunga kwenye Ligi ya NWSL baada ya awali kuwa Mtanzania wa kwanza kucheza katika ligi hiyo.
Kwenye mchezo huo ambao Washington iliongoza na kuruhusu Houston kusawazisha mara mbili, Clara aliingia na kufunga bao hilo akitokea benchi dakika ya 64 akichukua nafasi ya Melissa Bethi.
Clara anafunga bao hilo katika mechi yake ya pili kukipiga Washington baada ya mechi ya awali waliyofungwa bao 1-0 na Angel City ambapo pia aliingia dakika ya 64 akichukua nafasi ya Rosemonde Kouassi.
Mabao mengine ya Washington yalifungwa na Tara Rudd na Sofia Cantore wakati mabao ya Houston yaliwekwa kimiani na Miljana Ivanovic.
Washington inashika nafasi ya tatu kwa pointi 49 nyuma ya San Diego Wave yenye pointi 51 na vinara Gotham FC yenye pointi 55.
Mchezo unaofuata Washington itakuwa nyumbani Uwanja wa Audi kuumana na Gotham FC, Oktoba 17, mwaka huu.




