BASATA yatoa kauli shambulio la Zuchu
BARAZA la Sanaa la Taifa (BASATA) limelaani vikali kitendo cha kumshambuliwa kwa mawe, makopo kwa msanii Zuhura Othuman ‘Zuchu’ wakati wa tamasha la Wasafi lililofanyika Mbeya Septemba 28, 2024.
Kwenye tamko hilo, Basata ilieleza kuwa tukio hilo halikubaliki kwenye shughuli za sanaa nchini, kwa sababu linakiuka misingi ya heshima, utu, na mshikamano unaopaswa kuzingatiwa na wasanii na wadau wa sanaa.
Baraza limesisitiza umuhimu wa kuhakikisha usalama na mazingira ya amani kwa wasanii wanapokuwa kazini hasa wakati wa kutumbuiza wawapo jukwaani.
Aidha, Basata imetoa wito kwa wadau wa sanaa, ikiwa ni pamoja na waandaaji wa matukio, kuepuka migongano isiyo na tija na kushikamana katika kukuza sanaa yenye maadili na kuheshimu utu wa wasanii.
Tamko hili linaonesha msimamo wa baraza hilo katika kutetea na kulinda haki za wasanii, huku likitoa wito kwa mashabiki na waandaaji wa matukio kuwa waangalifu na kutunza usalama wa wasanii ili kuendeleza sanaa kwa njia ya ustaarabu.
Hii ni hatua muhimu katika kuhakikisha kwamba mazingira ya kazi ya wasanii yanakuwa salama na yenye heshima.
Msanii Barnaba ni miongoni mwa wasanii waliochukizwa na kitendo hicho na kuwa omba mashabiki kuwaheshimu wasanii wanapokuwa kazini.