Guardiola: Majeraha sio majanga ni changamoto tuu

MANCHESTER, Kocha wa Manchester City Pep Guardiola amesema anaamini kikosi chake kuandamwa na majeraha sio majanga bali changamoto tu zinazopima upana wa kikosi chake na ubora wa uwezo wake wa kukinoa kikosi hicho.
Akizungumza katika mkutano na wanahabari kuelekea mchezo wa kesho dhidi ya Crystal Palace kesho jumamosi katika uwanja wa Etihad wakiwa na misheni maalumu ya kuhakikisha kikosi hicho kinapata nafasi kwenye michuano ya Ulaya hasa Champions League.
Mabeki wake wa kikosi cha kwanza Manuel Akanji, John Stones na Nathan Ake wamekosa mechi za siku za hivi karibuni ambapo pia ameongezeka mshambuliaji kinara Erling Haaland pamoja na Rodri anayekosekana kwa muda mrefu.
“Majeraha yanatokea muda wowote wa msimu unaweza kuyaona kama changamoto au tatizo dogo lakini sio janga. janga ni sehemu tulipo kwenye msimamo wa ligi. ninafuraha jinsi tulivyoweza kuhimili hali hii ngumu na kuwa hapa tulipo leo” – amesema Pep.
Man City watakuwa na kibarua kingine kigumu mbele ya Crystal Palace kesho majira ya saa 8 mchana Afrika Mashariki wakiitafuta nafasi ya michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya msimu ujao baada ya hali mbaya msimu huu iliyopelekea kushindwa kutetea taji la EPL walilotwaa mara 4 mfululizo.