Ancelotti: Tumvumilie Mbappe
KOCHA mkuu wa mabingwa watetezi wa Ligi ya Mabingwa barani Ulaya Real Madrid, Carlo Ancelotti amesema mshambuliaji wake Kylian Mbappe anahitaji muda zaidi ili kuzoea mazingira ya klabu hiyo na kufanya vizuri.
Kylian Mbappe alionesha kiwango cha kufedhehesha na cha kukatisha tamaa kwa Real Madrid jana Jumatano, akishindwa kabisa kuisumbua safu ya ulinzi ya Liverpool na kukosa penalti katika kipigo chao cha 2-0 kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya Uwanjani Anfield.
Mfaransa huyo amekuwa na mwanzo mgumu Real Madrid baada ya kujiunga nao kutoka PSG mwezi Juni mwaka huu, akiwa na bao moja pekee katika mechi tano za UEFA akiwa na mabingwa hao wa Hispania.
Mshambuliaji huyo aliyeshinda Kombe la Dunia mwaka 2018 amefunga bao moja katika mechi zake sita zilizopita katika michuano yote lakini, Carlo Ancelotti alimtetea na kusema kuwa ni mchezaji “wa kipekee” ambaye anahitaji tu kuungwa mkono na uvumilivu ili ‘awake’ nchini Hispania.
“Ni wakati mgumu kwake, lazima tumuunge mkono na kumuonesha upendo wetu, tunaamini atakuwa sawa,”
“Inawezekana anakosa kujiamini. Wakati mwingine kuna mambo hayakuendei sawa. Watu hukosa penati, inatokea sana. Huwezi kuendelea kumhuzunisha.”
“Anajituma, lazima aendelee kujituma na kupambana. atazipita nyakati hizi. Mambo hayamwendei kwa sasa. Tunapaswa kuwa na subira tumuunge mkono na tumuoneshe upendo.” alisema Ancelotti.