Amorim: Liverpool ? hapana!
BAADA ya tetesi kuwa kocha wa Sporting Lisbon, Ruben Amorim amekubaliana na Liverpool kuifundisha msimu ujao, Mreno huyo amekanusha kuchukua mikoba ya Jurgen Klopp.
Ripoti za mapema wiki hii zilidai kuwa kocha huyo Mreno alikubali kuhamia Anfield msimu huu wa joto.
Amorim, 39, hataki kusikia tetesi hizo hata hivyo ametaka kuachwa kwanza wakati anaendelea kupambana katika michezo ya ligi.
“Hakukuwa na mahojiano na klabu yoyote, hakuna makubaliano na klabu yoyote,” alisema Amorim. “Hii ni mara ya mwisho nitazungumza kuhusu maisha yangu ya baadaye.”
Aliongeza: “Kitu pekee ambacho sote tunataka ni kuwa mabingwa na Sporting. Hakuna kitakachobadilika.”
Sporting wako kileleni mwa msimamo wa ligi na wana faida ya pointi nne zaidi ya wapinzani wao Benfica.