Zirkzee amkingia kifua Onana

LYON, MSHAMBULIAJI wa manchester United Joshua Zirkzee amemkingia kifua Golikipa wa klabu hiyo Andre Onana baada ya makosa binafsi ya Golikipa huyo kuigharimu ushindi klabu kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza wa robo fainali ya Europa League dhidi ya klabu ya Ligue 1 ya Lyon hapo jana akiita ukosoaji dhidi ya Onana ‘upuuzi’
Onana analaumiwa kwa makosa yaliyopelekea United kutoa sare ya 2-2 katika mchezo ambao awali ulitawaliwa na vijembe baina ya Onana na kiungo wa Lyon Nemanja Matic. Onana alidai United ni Bora ‘mara elfu’ ya Lyon huku Matic akisema golikipa huyo ndiye ‘Golikipa mbovu zaidi kwenye historia ya United’ ambayo amewahi kucheza.
Onana mwenye miaka 29 hakufanya kazi ya ziada kumziba mdomo Matic baada ya kushindwa kuzuia ‘free-kick’ ya Thiago Almada iliyotinga wavuni moja kwa moja kisha kuutema mpira wa Georges Mikautadze uliompata Rayan Cherki aliyeisawazishia Lyon dakika za jioni kisha ubao kusoma 2-2.
Alipoulizwa kuhusu uchezaji wa Onana na ukosoaji anaopata kutoka kwa mashabiki Zirkzee alisema anaungana na kocha wake Amorim ambaye alisema kosa la mchezaji ni kosa la timu na kusema kuwa ni upuuzi kumlaumu Onana pekee wakati iliyopoteza ni timu nzima.
“Ndio 100% sisi ni timu moja hatutamtoa mtu yeyote kwa sababu amefanya kosa kumlaumu Onana ni Upuuzi japo kupata sare kama hivi kidogo inaumiza lakini sitaki kusema inmetuchanganya. tunapaswa kuangalia mchezo wa nyumbani si kunyoosheana vidole, tuna mchezo dhidi ya Newcastle kisha tutarudiana tena nyumbani wiki ijayo”
Europa League ndio tumaini pekee kwa United baada ya mwendo usioridhisha kwenye Ligi Kuu ya England bila shaka wana matumaini ya kubeba kombe hilo ili kujinusuru na kelele za mashabiki.