Ahmed: Kibu D hatuumizi kichwa
MOROGORO: MENEJA wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally amesema kitendo cha utovu wa nidhamu wa mshambuliaji wao, Kibu Denis kutokuwepo kambi hakutathiri mipango ya kocha, Fadlu Davids.
Amesema kitendo cha kutokuwepo kambini hadi sasa ni utoro kambini na watamchukulia hatua za kinidhamu kwa kosa la kutokuwasili kambini kwa ajili ya maandalizi ya msimu ujao.
Ikumbukwe kwamba mchezaji huyo aliongezewa mkataba na klabu hiyo wa miaka miwili zaidi utakaoisha Juni 2026 na kumlipa stahiki zake za kimkataba.
Ahmed amesema kutokuwepo kwa Kibu hakuathiri program za kocha kwa sababu wamefanya usajili kulingana na mahitaji ya timu.
“Kibu hadi sasa hajaungana na kikosi cha timu hiyo nchini Misri walipoweka kambi kwa ajili ya maandalizi ya msimu wa Mashindano.
Tulimuongeza mkataba wa miaka miwili na amesaini kuitumikia Simba, tumemlipa fedha zote na mahitaji yote aliyohitaji. amelipwa kama kondakta fedha alikabidhiwa mkononi na kuondoka, kama taasisi ya Simba hatuna deni na mchezaji bali Simba inamdai utumishi wake,” amesema Ahmed.
Ameeleza kuwa baada ya kumaliza kwa ligi alienda Marekani wakampa taarifa ya kambi, kupima afya na safari ya Misri. Baadae aliwaambia hati ya kusafiria imejaa.
“Kweli alirudi na kufatilia hati yake lakini hakutokea ofisini kwa ajili ya safari, alipotafutwa kwa ajili ya kuleta passport akasema ameenda Kigoma, baada ya hapo zimeanza danadana za hapa na pale, tutaendelea kumtafuta lakini jana tulisikia ameenda nje ya nchi,” amesema meneja huyo.
Kuhusu kupata timu nje , Ahmed ameeleza kuwa hawafahamu na hilo jambo lingekuwepo angetoa taarifa kwa sababu sera ya Simba kuruhusu mchezaji akipata malisho mema .