Zakazakazi hana siri, aweka silaha za ushindi hadharani

DAR ES SALAAM: UONGOZI wa Azam FC, umeingia makubaliano ya mwaka mmoja ya ushirikiano na timu ya mpira wa miguu ya wanawake ya Fountain Gate Princess, ikiwa ni kutekeleza kanuni na sheria ya Shirikisho la soka Afrika (CAF) kwa klabu inayoshiriki michuano ya kimataifa.
Azam FC inaungana na Yanga kuwakilisha nchi kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa msimu wa 2024/25 baada ya kumaliza nafasi ya pili Ligi Kuu Bara msimu wa 2023\24.
Akizungumza na Spotileo, Ofisa Habari wa Azam FC, Zakaria Thabiti ‘Zaka’, amesema makubalino hayo ni kukidhi kanuni ya CAF iliyoanza kutumika msimu uliopita inayozitaka timu zinazoshiriki michuano ya Afrika kuwa na timu za wanawake au kushiriki katika uendeshaji na taasisi nyingine yenye uendashaji wa soka hilo.
Amesema wameona bora kuingia makubaliano na fountain Gate Princess baada ya msimu uliopita kuingia mkataba kama huo na Baobab Queens tayari umefikia kikomo na kushuka daraja.
“Kwa makubaliano haya rasmi sasa Fountain Gate Princess ambayo maskani yake yapo jijini Dodoma, itakuwa ni klabu dada ya Azam FC kuanzia msimu ujao, kwa kufuata kanuni na sheria ya CAF. Msimu ujao tumedhamiria kufanya vizuri na hatutaki kurudia makosa ya nyuma,” amesema.
Amesema kwenye anga la kimataifa wanaimani watafanya kitu kikubwa ambacho kitawashangaza wengi wasiokuwa na imani na timu hiyo hali ya kuwa msimu ujao wamedhamiria kucheza makundi na kuweka rekodi ya kwenda robo fainali.
“Tumecheza michuano ya kimataifa mara kadhaa tukiishia hatua za awali, msimu wa 2024/25 tumejipanga vizuri hatuhitaji kurudia makosa ya nyuma, tulianza msimu kwa mpango kazi hakuna aliyetarajia kama tutakuwa hapa na imetokea na tunaenda kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika.
Hatutaishia kama ilivyokuwa miaka ya nyuma, tunaenda kushiriki, kuonyesha upinzani mkubwa,tunakwenda kwenye anga la kimataifa tutafanya vizuri kwa kuwa mipango ipo vizuri ikiwemo suala la usajili na kambi maalum ya Pre Season.” amesema Zaka.
Ameongeza kuwa suala la usajili linaendelea kufanyika kulingana na mahitaji ya benchi la ufundi kuimarisha na kuongeza nguvu kwenye madhaifu kwa ajili ya kwenda kushinda katika michuano ya kimatifa.
Zaka amesema kutokana na mipango hiyo ya kufanya vizuri , wamejiondoa kwenye mashindano ya Kagame ili kupata muda wa kufanya maandalizi mazuri na kuwapa muda wachezaji wapya na waliosalia kuzoeana.