Fadlu: Hatujajipata bado ila tutapiga mtu
DAR ES SALAAM: KUELEKEA mchezo wa dabi dhidi ya Yanga, Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids amesema bado ana changamoto kwenye safu ya ulinzi lakini amejipanga vizuri namna ya kuwazuia Yanga kwenye mchezo wa nusu fainali wa Ngao ya Jamii.
Amesema anafahamu Yanga wako vizuri katika kushambulia na amefanyia kazi ubora wa eneo hilo kwa kuisuka imara safu ya mabeki wake na wapo tayari kukabiliana na wapinzani siku ya kesho uwanja wa Benjamini Mkapa, jijini.
Simba ni mabingwa watetezi wa Ngao ya jamii baada ya msimu uliopita kuibuka na ushindi wa penati 3-1 dhidi ya Yanga katika mchezo wa fainali ya kombe hilo, uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
“Timu yangu mpya tumejipanga vizuri, tunaichukulia mechi hii kama zilivyo nyingine na tunahitaji kushinda ili kuanza vizuri msimu kwa kuleta kombe hili. Nina uzoefu wa michezo mikubwa ya derby, ukiangalia timu yetu ni mpya hivyo tutakuja na mbinu tofuti kuhakikisha tunapata matokeo mazuri,” amesema.
Naye Nahodha wa Simba, Mohammed Hussein ‘Zimbwe Jr’, amesema wamekuwa na maandalizi mazuri, wamezungumza na wachezaji wenzao wapya kuwaeleza ukubwa wa mechi na muda waliokuwepo pamoja unatosha kukabiliana na Yanga.
“Kulingana na maandalizi tuliyofanya, timu yetu imeimarika zaidi ila tunaamini tunaenda kukutana na timu yenye wachezaji wazuri. Utakuwa mchezo wenye ushindani ila malengo yetu ni kupata ushindi kesho,” amesema Zimbwe Jr.
Mchezo huo wa Ngao ya Jamii ni sehemu ya ufunguzi wa msimu wa Ligi Kuu Bara unaotarajiwa kuanza kutimua vumbi Agosti 16 mwaka huu katika viwanja mbalimbali nchini Tanzania.