Ligi Kuu

Yanga yaelekea Zanzibar, yatangaza viingilio

DAR ES SALAAM: KIKOSI cha Yanga kimeelekea Zanzibar kwa ajili ya kuweka kambi ya mwisho ya maandalizi ya mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya MC Alger ya Algeria utakaochezwa Jumamosi, Novemba 28, mwaka huu.

Yanga itacheza mchezo huo kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, saa 10:00 jioni, ikiwa na jukumu la kuanza vizuri kampeni yake ya Kundi B, ambalo pia lina Zamalek ya Misri na Club Africain ya Tunisia.

Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ali Kamwe, amesema benchi la ufundi pamoja na baadhi ya viongozi wa menejimenti wameanza safari kuelekea Zanzibar ili kuipa timu nafasi ya kujiandaa kwa takribani siku nne kabla ya kukutana na wapinzani hao.

“Maandalizi hayo yatahusisha siku za Jumanne, Jumatano, Alhamisi na Ijumaa, huku klabu ikitambua umuhimu wa mchezo huo katika kuanza safari ya kuwania kufuzu hatua ya robo fainali, tunaomba mashabiki mjitokeze kwa wingi Jumamosi kuisapoti timu,”amesema.

Katika hatua nyingine, Kamwe ametangaza viingilio vya mchezo huo huku akieleza kuwa klabu imeboresha mfumo wa ununuzi wa tiketi kwa kushirikiana na kampuni ya Lipa Financial Solutions ili kuondoa usumbufu wa kupanga foleni vituoni.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button