Swae Lee asimamisha onesho lake baada ya kumwagiwa bia jukwaani

MAREKANI: MSANII maarufu wa muziki wa Hip Hop nchini Marekani, Swae Lee, amezua gumzo baada ya kusimamisha onesho lake wakati akitumbuiza katika tamasha la Cherry Blossom Festival nchini India, kufuatia kurushiwa kinywaji aina ya bia kilichompiga usoni akiwa jukwaani.
Tukio hilo lilitokea eneo la Madan Kurkalang Sports Complex, mjini Shillong, jimbo la Meghalaya, ambako msanii huyo alikuwa akitumbuiza mbele ya mashabiki waliojitokeza kushuhudia tamasha hilo.
Video zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii zilimuonesha Swae Lee akishtuka baada ya kinywaji hicho kumfikia usoni, kisha kuamuru muziki usimamishwe huku akitaka kufahamu mtu aliyerusha kinywaji hicho. Baadaye aliitisha walinzi wake kumtafuta mtu aliyehusishwa na tukio hilo.
Kwa mujibu wa taarifa zilizoripotiwa na vyombo vya habari vya India, walinzi walimtoa mtu aliyedhaniwa kuhusika na tukio hilo nje ya eneo la tamasha. Hata hivyo, baadaye mtu mmoja aliyehusishwa na tukio hilo alijitokeza kukanusha madai hayo, akisema alituhumiwa kimakosa na kuonesha video aliyodai kuthibitisha kuwa hakuwa na kikombe kilichotumika kurushia bia.
Akizungumzia tukio hilo kupitia video alizochapisha kwenye ukurasa wake wa Instagram, Swae Lee alisema hakufahamu kama kitendo hicho kilifanyika kwa makusudi au kwa bahati mbaya, lakini alikerwa na hali hiyo kwa kuwa kinywaji kilimwingia hadi puani. Hata hivyo, alisisitiza kuwa hakutaka tukio hilo lifute furaha ya onesho zima.
Licha ya tukio hilo, msanii huyo aliendelea na onesho lake hadi mwisho na kuwasifu mashabiki wa India kwa mapokezi mazuri. Alieleza kuwa alikuwa na wakati mzuri katika tamasha hilo na kwamba tukio hilo lilikuwa la mtu mmoja, huku akisisitiza umuhimu wa mashabiki kuheshimu wasanii wanapokuwa jukwaani.




