Mastaa

Lulu na Ray C wampongeza Zuchu kwa ukarimu kwa Davido Chioma

DAR ES SALAAM: WASANII wa filamu na muziki, Elizabeth Michael ‘Lulu’ na Rehema Chalamila ‘Ray C’, wamempongeza mwanamuziki Zuhura Othuman ‘Zuchu’ kwa kuonyesha ukarimu na kuthamini mila na desturi za Kitanzania baada ya kuwahudumia nyumbani kwake msanii wa Nigeria, Davido, na mkewe, Chioma.

Zuchu amezungumziwa na baadhi ya watu kwenye mitandao ya kijamii baada ya kuonekana akitimiza majukumu ya kuwahudumia wageni hao nyumbani kwake, jambo ambalo limeibua mjadala kuhusu nafasi ya mwanamke katika familia na namna ya kuwapokea wageni.

Akitoa maoni yake, Elizabeth Michael amemtetea Zuchu dhidi ya wanaomkosoa kwa kitendo hicho, akisisitiza kuwa kuwahudumia wageni nyumbani si jambo la kulaumiwa, bali ni sehemu ya ukarimu na ustaarabu.

Elizabeth amesema: “Kama kuhudumia wageni kwako ni tatizo, basi bado hawajakutana na type yake. Ikichelewa ugenini, ninasadia kazi.”

Kwa upande wake, Ray C pia amempongeza Zuchu, akivutiwa na namna alivyoweza kutofautisha maisha yake ya umaarufu jukwaani na majukumu yake anapokuwa nyumbani.

“Mwanamke aliyefundwa utamjua tu kwa matendo yake! Kauvua umaarufu wa stejini, kauvaa uhusika wa nyumbani kama mke mbele ya wageni,” amesema Ray C.

Ameongeza kuwa kitendo hicho kinaakisi maadili ya Kitanzania ya kumkaribisha na kumjali mgeni anapofika nyumbani.

Pongezi hizo za wasanii hao zimeongeza mjadala kuhusu ukarimu, heshima na namna Zuchu alivyowapokea wageni wake, huku wakisisitiza kuwa kuwahudumia wageni ni sehemu ya utamaduni wa Watanzania.

Related Articles

Back to top button