Kwingineko

Cristiano Ronaldo aingia rasmi katika utengenezaji wa vipindi vya TV

URENO: MSHAMBULIAJI nyota wa Ureno na klabu ya Al-Nassr, Cristiano Ronaldo, ameanza ukurasa mpya katika maisha yake nje ya soka baada ya kutangaza kuanza kwa utengenezaji wa kipindi chake cha kwanza cha televisheni kinachoitwa Day 1s.

Ronaldo alitangaza hatua hiyo kupitia akaunti yake ya Instagram, akiandika: “Habari za kusisimua! Uzalishaji wa kipindi changu cha kwanza cha televisheni, Day 1s, umeanza rasmi. Mengi zaidi yanakuja.” Tangazo hilo limeibua matarajio miongoni mwa mashabiki wake wanaotaka kumuona katika tasnia ya burudani.

Kipindi hicho kinahusu ulimwengu wa soka, hususan maisha ya mawakala wanaosimamia wachezaji, biashara za usajili na mikataba mikubwa inayohusisha klabu mbalimbali. Simulizi yake inamzungumzia wakala wa kubuniwa wa Uingereza anayeitwa Stanley Dalton.

Mwigizaji Damian Lewis, anayefahamika kupitia tamthilia za ‘Homeland ‘ na ‘Billions’, ndiye anayeigiza mhusika Stanley Dalton. Vilevile, nyota wa zamani wa soka Thierry Henry na mwanamuziki wa Uingereza Dave wametajwa kuhusishwa na mradi huo.

Ronaldo anashiriki katika utayarishaji wa kipindi hicho kupitia kampuni ya UR·MARV Studios, aliyoianzisha kwa ushirikiano na mtayarishaji na mwongozaji maarufu wa filamu ambaye ni raia wa Uingereza, Matthew Vaughn, anayefahamika kwa kazi zake za filamu za Kingsman. Mradi huo pia unatarajiwa kumfungulia Ronaldo nafasi mpya ya kujihusisha na uigizaji.

Hata hivyo, hadi sasa tarehe rasmi ya kuanza kuoneshwa, idadi ya vipindi na kituo au jukwaa litakalorusha Day 1s havijatangazwa. Hatua hiyo inaonesha namna Ronaldo anavyoendelea kupanua shughuli zake za kibiashara na burudani nje ya uwanja wa soka.

Related Articles

Back to top button