Ruby aaga Bongo fleva sasa kumtumikia Mungu

DAR ES SALAAM: MSANII wa muziki wa Bongo Fleva, Hellena George ‘Ruby’, ametangaza rasmi kuachana na muziki wa kidunia na kuelekeza nguvu zake katika kuimba nyimbo za Injili pamoja na kuhubiri Neno la Mungu.
Ruby, ambaye jina lake halisi ni Hellen George, amesema uamuzi huo umetokana na hali ya kutokuwa na amani ya ndani aliyokuwa akiipitia katika kipindi chote alichokuwa akifanya muziki wa Bongo Fleva.
Amesema licha ya kuwa sehemu ya tasnia hiyo, hakuwahi kujisikia huru kikamilifu, huku nafsi yake ikiendelea kumhukumu, jambo lililomfanya kutafakari upya mwelekeo wa maisha yake na hatimaye kuamua kumrudia Mungu.
Akieleza sababu za kuchukua uamuzi huo, Ruby amesema “Sasa naamini umefika wakati wa kuachana na muziki wa kidunia na kutumia kipaji chake kumtumikia Mungu kupitia nyimbo za Injili na kuhubiri.
Katika kuonesha dhamira yake mpya, msanii huyo amefuta katika ukurasa wake wa Instagram maudhui yote ambayo hayaendani na misingi ya maisha yake mapya ya kiroho.
Aidha, Ruby amebainisha kuwa kuanzia sasa atajikita katika huduma ya uimbaji wa Injili na kuhubiri Neno la Mungu, huku akiomba kupata mialiko katika ibada na makanisa mbalimbali ili kutoa huduma hiyo.
Uamuzi huo unaashiria mwanzo mpya katika safari yake ya muziki, safari ambayo sasa amesema anataka kuitumia kumtumikia Mungu badala ya kuendelea na muziki wa kidunia.




