Mwanariadha wa Kenya afariki dunia

NAIROBI: MWANARIADHA wa Kenya, David Chelule, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 49, taarifa zilizothibitishwa na Shirikisho la Riadha nchini Kenya (Athletics Kenya).
Chelule, ambaye alikuwa bingwa wa mbio za nyika za dunia kwa vijana chini ya miaka 20 mwaka 1996, alifariki Ijumaa, Novemba 6, 2026.
Katika salamu zake za rambirambi, Athletics Kenya ilimtaja marehemu kama mwanariadha aliyeiweka Kenya katika ramani ya kimataifa kupitia mafanikio yake katika mbio za masafa ya kati na marefu.
Shirikisho hilo lilisema kujituma, kipaji na kujitolea kwake katika riadha kutabaki kuwa sehemu muhimu ya historia ya michezo nchini Kenya.
Chelule aliandika historia mwaka 1996 baada ya kutwaa medali ya dhahabu katika mbio za kilomita nane kwa vijana chini ya miaka 20 kwenye mashindano ya Dunia ya Mbio za Nyika yaliyofanyika Stellenbosch, Afrika Kusini.
Mwaka huohuo, alitwaa medali ya fedha katika mbio za mita 5,000 kwenye Mashindano ya Dunia ya Riadha kwa Vijana yaliyofanyika Sydney, Australia.
Mwaka 1999, alitwaa ubingwa wa kitaifa wa mbio za mita 10,000 kwa kutumia dakika 28:37.5.
Miongoni mwa mafanikio mengine ya Chelule ni ushindi katika mashindano ya Torino Nebiolo Day mwaka 2000 katika mbio za mita 3,000, Le-Puy-en-Velay mwaka 2002 katika kilomita 15, Prato Half Marathon mwaka 2006 na Milano 10km mwaka 2007.
Mashindano yake ya mwisho ya ushindani yalikuwa Brescia Marathon mwaka 2010, ambapo alishinda baada ya kutumia saa 2:13:53.
Shirikisho la Riadha nchini Kenya limesema kifo chake ni pigo kubwa kwa familia ya riadha nchini Kenya na kimataifa.




