Chalamila kuiongoza hamasa ya Serengeti Boys Qatar

DAR ES SALAAM: MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amesema atakwenda nchini Qatar kuishangilia timu ya Taifa ya vijana chini ya miaka 17 (Serengeti Boys) katika moja ya mechi zake za Fainali za Kombe la Dunia zitakazoanza Novemba 19 hadi Desemba 13 mwaka huu.
Chalamila amesema mbali na kwenda mwenyewe kuipa moyo timu hiyo, pia kuna mpango wa kugharamia safari ya baadhi ya mashabiki watakaokwenda Qatar kushuhudia na kuishangilia Serengeti Boys katika mashindano hayo.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam leo, Chalamila amewataka Watanzania kuungana na Serikali katika kuiunga mkono timu hiyo, akieleza kuwa ushiriki wake katika mashindano hayo ni mafanikio makubwa kwa soka la vijana nchini.
Serengeti Boys imepata nafasi ya kushiriki mashindano hayo baada ya kufanya vizuri katika Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya miaka 17 (AFCON U17) zilizofanyika Morocco mwaka huu, ambako ilifika fainali na kupoteza kwa mikwaju ya penalti dhidi ya Senegal baada ya sare ya bao 1-1 katika muda wa kawaida.
Katika Kombe la Dunia, Tanzania imepangwa Kundi I pamoja na Brazil, Jamhuri ya Ireland na Costa Rica, huku ikitarajiwa kutumia nafasi hiyo kupima uwezo wake dhidi ya mataifa yenye historia kubwa katika soka la kimataifa.
Chalamila amesema mafanikio hayo yanaonesha matunda ya uwekezaji unaofanywa na Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan katika sekta ya michezo, hivyo ametoa wito kwa Watanzania kuwa wazalendo na kuipa timu hiyo hamasa.



