Abuya arejea mazoezini Yanga

DAR ES SALAAM: KIUNGO wa Yanga, Duke Abuya, ameanza mazoezi jana baada ya kukaa nje ya uwanja kwa muda akiuguza jeraha la nyama za paja alilolipata katika mchezo wa dabi dhidi ya Simba.
Kurejea kwa Abuya mazoezini ni hatua muhimu kwa Yanga katika kuimarisha kikosi chake, huku mchezaji huyo akitarajiwa kuendelea na programu ya mazoezi chini ya benchi la ufundi ili kurejesha utimamu wake.
Abuya alipata jeraha hilo Oktoba 10, mwaka huu, wakati Yanga ilipokutana na Simba katika mchezo wa Ligi Kuu uliomalizika kwa Simba kuibuka na ushindi wa mabao 2-1.
Kiungo huyo alishindwa kuendelea na mchezo baada ya kupata maumivu, hali iliyomlazimu kutoka uwanjani na nafasi yake kuchukuliwa na mchezaji mwingine.
Awali, taarifa kuhusu hali yake zilieleza kuwa angeweza kukaa nje kwa kipindi cha wiki mbili hadi tatu, huku kurejea kwake kukitegemea maendeleo ya matibabu na hali yake ya kiafya.
Hata hivyo, kuanza mazoezi jana kunaashiria hatua nzuri katika kurejea kwake, ingawa bado haijathibitishwa ni lini atakuwa tayari kucheza mechi za ushindani.
Aidha, beki Yao Kwasi naye pia amerejea mazoezini ikiwa ni ishara njema kuelekea kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo Yanga itahitaji kikosi kipana kwa ajili ya ushindani wa wapinzania walioko mbele yao.




