Kiduku: Nimerudi kwa nguvu mpya

DAR ES SALAAM: BONDIA Twaha Kiduku ametangaza kurejea ulingoni Novemba 13 mwaka huu, akisema kipindi alichokaa nje ya ulingo kwa takribani mwaka mmoja kilikuwa sehemu ya maandalizi ya kurejea akiwa na nguvu mpya na kuonesha uwezo wake kwa mashabiki.
Kiduku, ambaye pambano lake la mwisho lilikuwa Julai 26, 2025 dhidi ya Alick Mwenda, alishinda kwa Technical Knockout (TKO) katika raundi ya tatu, akitetea heshima yake katika pambano la kuwania ubingwa wa Tanzania uzito wa Super Middleweight.
Baada ya kukaa nje kwa kipindi hicho Kiduku amesema sasa amejipanga kurejea kwa kishindo huku akiwataka mashabiki wake kujiandaa kwa burudani.
“Kimya changu hakikuwa mwisho wa safari, bali kilikuwa sehemu ya maandalizi ya kurudi kwa nguvu mpya. Nimejifunza mengi, nimejipanga na sasa muda wa kuzungumza umefika mwisho. Ni muda wa kuonesha kazi ndani ya ulingo.
“Mungu akipenda, Novemba 13 narudi kwa kishindo. Mashabiki wangu jiandaeni kwa burudani. Kumbukeni, bondia wa kweli hapimwi kwa maneno yake, bali kwa kile anachokionesha ulingoni,” amesema Kiduku.
Kukaa huko nje kwa muda kumeshusha nyota ya mchezaji huyo katika viwango vya ubora wa kimataifa hivyo, anahitaji mapambano makubwa yenye hadhi kurudisha heshima yake.




