Nyumbani

Yanga hakuna kulala, makali yanatafutwa

DAR ES SALAAM:WAKATI ushindani wa soka ukiendelea kupanda, wachezaji wa Yanga wameonekana kutotaka kuacha nafasi yoyote katika kujiimarisha kimwili na kurejesha makali yao, wakitumia programu za ziada za mazoezi chini ya mkufunzi binafsi maarufu Denzel Trainer.

Miongoni mwa nyota walioonekana kwenye programu hiyo ni Stephane Aziz Ki, Hussein Zakouani na Cheikh Toure, ambao wamekuwa wakifanya mazoezi maalumu kwa lengo la kuongeza uimara wa mwili, kasi na utimamu unaohitajika katika ushindani wa soka la kisasa.

Hatua hiyo inaonesha namna wachezaji wanavyozidi kutambua umuhimu wa kujiongezea ubora nje ya programu za kawaida za klabu, hasa katika kipindi ambacho kila mchezaji anahitaji kuwa katika kiwango cha juu ili kupata nafasi na kudumu kwenye kikosi.

Denzel Trainer amekuwa miongoni mwa makocha binafsi wanaotumiwa na wachezaji mbalimbali wa soka nchini wanaotafuta kuongeza nguvu, uimara na kurejesha makali yao.

Si mara ya kwanza kwa wachezaji wenye majina makubwa kutumia programu zake. Waliowahi kupitia mikononi mwake ni pamoja na Pacome Zouzoua na Yao Kouassi, ambao pia wametumia mazoezi ya ziada katika safari zao za kuimarisha uwezo wao.

Hata upande wa watani wao Simba, wachezaji kama Elly Mpanzu, Clatous Chama na Ibrahim Doumbia ni miongoni mwa majina yaliyowahi kuhusishwa na programu za mazoezi za mkufunzi huyo.

Kwa upande wa Yanga, kuonekana kwa Aziz Ki, Zakouani na Toure katika mazoezi hayo kunaweka wazi kiu ya wachezaji kuendelea kujiimarisha na kutafuta kiwango bora zaidi.

 

Related Articles

Back to top button