Maema hana wasiwasi na Simba hii

DAR ES SALAAM: KIUNGO wa kati wa Simba SC, Neo Maema licha ya kukiri kuwa ligi imezidi kuwa ngumu lakini hana wasiwasi na ubora na upambanaji wa wachezaji wenzake kwenye kutafuta pointi tatu muhimu.
Maema amezungumza hayo baada ya ushindi wa mabao 3-2 walioupata Simba wakitokea nyuma dhidi ya Namungo kwenye mchezo uliopigwa jana Jumatatu Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Maema alisema kasi yao ilipungua baada ya kutangulia kufunga bao la kwanza, kitu kilichowapa nguvu wapinzani wao, waliorudi mchezoni na kufunga mabao mawili.
“Kusema kweli hata hivyo, nimefurahishwa na uthabiti na roho ya kupambana iliyooneshwa na timu nzima.
“Maana kadri tunavyocheza mechi, ndivyo wapinzani wanavyozidi kuwa wagumu; kwa hivyo, mambo hayawi rahisi kamwe. Muhimu zaidi ni kupata pointi tatu mwisho mwa siku.
“Pia, shukrani kwa mashabiki waliojitokeza kwa wingi. Kama nilivyosema, haitakuwa rahisi kamwe, hii ni mechi ya kumi msimu huu na tumeshinda zote, hivyo tunamshukuru Mungu,” alisema Maema raia wa Afrika Kusini.
Ameeleza kuwa endapo watatumia fursa walizonazo, vipaji walivyopewa, na kudumisha umoja baina ya wachezaji na bila kujali changamoto zitakazojitokeza basi anaamini msimu huu watafanikiwa mno.
Simba imezidi kujikita kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na pointi 30 baada ya mechi 10, ikiwaacha wapinzani wao, Yanga katika nafasi ya pili kwa pointi 25 baada ya mechi 10 pia.




