Mzize: Goli limenipa morali

DAR ES SALAAM: MSHAMBULIAJI wa Yanga, Clement Mzize, amesema bao alilofunga jana dhidi ya Mashujaa limempa morali ya kuendelea kufanya vizuri.
Mzize aliingia kipindi cha pili timu ikiwa na bao 1-1 na yeye kuifungia timu bao la pili na kuibuka na ushindi wa mabao 2-1, ikiwa ni bao lake la kwanza msimu huu tangu atokee majeruhi.
Mshambuliaji huyo ndiye aliyeibuka nyota bora wa mchezo huo ambapo amesema amefurahia kurejea salama na kufunga bao baada ya muda mrefu, akieleza kuwa mafanikio hayo yametokana na juhudi alizokuwa akifanya mazoezini.
Amesema alikuwa akiamini kuwa siku moja angepata nafasi ya kufunga na kurejea katika kiwango chake, hivyo bao hilo limempa motisha ya kuongeza bidii katika michezo inayofuata.
“Nashukuru Mungu kwa kurejea salama. Bao langu la kwanza msimu huu limenipa morali kubwa kwa sababu nimekuwa nikilifanyia kazi sana mazoezini. Ninaamini nitaendelea kufanya vizuri kila nitakapopata nafasi ya kucheza,” amesema.
Mzize amewashukuru mashabiki wa Yanga kwa kuendelea kumuunga mkono wakati wote aliokuwa nje ya kiwango alichotarajia, akisema hajapoteza imani nao na anaahidi kuendelea kupambana kwa ajili ya timu hiyo.
Amesema anaamini bado ana nafasi ya kuboresha kiwango chake kadiri ligi inavyoendelea, huku akiahidi kufanya vizuri zaidi katika michezo ijayo ili kuwalipa mashabiki waliomsubiri kwa muda mrefu.




