Singida Black Stars yajipanga kukabiliana na ratiba ngumu

MWANZA: MENEJA Habari na Mawasiliano wa Singida Black Stars, Hussein Massanza, amesema kikosi hicho kimejipanga kukabiliana na ratiba ngumu ya michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara, huku kikiwa na jukumu la kutafuta matokeo mazuri katika mechi zinazofuata.
Massanza amesema timu hiyo tayari imewasili Mwanza kwa ajili ya mchezo dhidi ya Pamba Jiji utakaochezwa Alhamisi, kabla ya kuikabili Mbeya katika mchezo mwingine unaotarajiwa kufanyika Novemba 2.
Amesema licha ya kuwa na michezo inayofuatana kwa muda mfupi, benchi la ufundi chini ya kocha mkuu limejipanga vizuri, likifahamu namna ya kutumia kikosi chake na kufanya mabadiliko yatakayosaidia wachezaji kukabiliana na mzigo wa michezo hiyo.
Ameeleza kuwa kocha atatathmini hali ya wachezaji na kuamua nani aanze na nani apumzishwe ili kuhakikisha timu inakuwa katika hali nzuri ya ushindani kwa kila mchezo.
Singida Black Stars inaingia katika michezo hiyo ikiwa na morali baada ya kuifunga Tusker FC ya Kenya na kufuzu hatua ya makundi ya mashindano ya Afrika.
Mafanikio hayo yanaipa timu hiyo hamasa ya kuendelea kupambana katika mashindano ya kimataifa na ligi ya ndani, huku ikilenga kupata matokeo mazuri katika ratiba yake inayofuata.




