Fikiri: Hasira zetu tutazimaliza kwa Kagera

TANGA: KOCHA Mkuu wa Coastal Union, Fikiri Elias, amesema kikosi chake kimejipanga kurejea kwenye matokeo mazuri kitakapokutana na Kagera Sugar katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaochezwa kesho.
Fikiri amesema baada ya kurejea Tanga wakitokea Ruangwa Lindi timu hiyo imefanya mazoezi ya kuondoa uchovu na kujiweka imara zaidi kwa ajili ya mchezo huo, huku ikilenga kutumia vizuri nafasi ya kucheza nyumbani ili kupata ushindi.
Coastal Union inaingia katika mchezo huo ikitoka kupoteza kwa mabao 2-1 dhidi ya Namungo katika mchezo uliopita wa ligi uliochezwa ugenini, matokeo yanayoifanya ihitaji kurejea kwenye ushindani kwa kupata pointi muhimu.
Hata hivyo, Fikiri amesema mchezo huo hautakuwa rahisi kwa kuwa Kagera Sugar nayo inahitaji matokeo mazuri kutokana na nafasi yake isiyoridhisha kwenye msimamo wa ligi, hivyo anatarajia ushindani mkubwa kutoka kwa wapinzani wao.
Amesisitiza umuhimu wa wachezaji wake kutumia vizuri maandalizi waliyoyafanya na kuonesha kiwango kizuri ili kufikia lengo la kuibuka na ushindi mbele ya mashabiki wao.
Kocha huyo pia amewataka mashabiki wa Coastal Union kujitokeza kwa wingi uwanjani kuisapoti timu hiyo na kuwapa wachezaji hamasa ya kupambana kupata matokeo mazuri katika mchezo huo.




