Coastal hasira zote Ligi Kuu
DAR ES SALAAM: KAIMU Kocha Mkuu wa Coastal Union, Ngawina Ngawina amesema wanaenda kwa tahadhari kubwa na kutafuta pointi tatu katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya KMC FC.
Amesema vijana wake wapo tayari na wamesahau matokeo ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAF), hasira zao watamalizia dhidi ya wapinzani wao hao ambao wanatumia uwanja wa nyumbani.
Jumapili, Agosti 25, Coastal Union iliaga rasmi mashindano ya CAF baada ya kukubali kichapo ya jumla ya mabao 3-0 dhidi ya FC Bravos Do Maquis ya nchini Angola na mechi ya maruadiano kutoka suluhu, Uwanja wa Azam Complex, uliopo Chamanzi.
Ngawina amesema vijana wake wapo tayari kwa mchezo huo na wamesahau matokeo ya michuano ya kimataifa na akili zao wanazielekeza katika mchezo huo ili kupata ushindi.
Amesema wanaingia dhidi ya KMC FC kwa tahadhari kubwa kwa sababu wanafahamu aina ya mchezo wanaocheza na wapo makini kukabiliana nao licha ya kucheza kucheza ugenini.
“Tumesahau mashindano ya kimataifa sasa akili zinarudi kwenye ligi kuu, tunatambua tuna mchezo mgumu lakini tumejipanga vizuri kukabiliana na wapinzani wetu,” amesema kocha Ngawina.
Mwakilishi wa wachezaji wa Coastal Union, Jackson Shiga, amesema wapo tayari dhidi ya KMC FC, utakuwa mchezo mzuri na wanahitaji kushinda mechi ya kwanza ya ligi na kuhamasisha kuendelea kufanya vizuri michezo ijayo.
“Hatutaki kuona makosa ya michuano ya kimataifa, yanajirudia kwenye mechi yetu ya kesho na michezo mwingine ya ligi, tupo tayari kuwaonesha mchezo mzuri na kutafuta pointi tatu,” amesema Shiga.