Mr Blue:Chanzo cha kuondoka Dudu Baya Foundation

DAR ES SALAAM:MSANII wa Bongo Fleva, Kheri Sameer Mr Blue, amefunguka kuhusu historia ya wimbo wake wa Gari la Baba, akieleza kuwa wazo la wimbo huo lilianza wakati akiwa chini ya lebo ya Dudu Baya Foundation.
Mr Blue amesema alipata wazo la kuandika wimbo huo kutokana na mazingira ya familia yake, ambapo alieleza kuwa upande wa baba yake ulikuwa na uwezo wa kifedha na baba yake alikuwa akimiliki gari.
Kwa mujibu wa Mr Blue, baada ya kupata wazo hilo alilipeleka kwa Dudu Baya, lakini hakulipokea na badala yake alimtaka atengeneze wimbo mwingine uliokuwa na dhana ya Mpangaji.
Msanii huyo amesema wakati huo aliona wazo la gari la baba lilikuwa rahisi kwake kulitengeneza kwa sababu alikuwa analifahamu vizuri hilo suala, tofauti na dhana ya Mpangaji, kwani hakuwahi kupanga nyumba.
“Baba yangu alikuwa na gari. Upande wa baba yangu walikuwa matajiri, nikapata idea ya kuingia na gari la baba.
Nilipompelekea Dudu Baya, akaniambia, ‘Baba yako ana gari?’ Akaniambia nitengeneze ngoma nyingine inaitwa Mpangaji. Mimi sijawahi kupanga nyumba, na Dudu Baya Foundation nikatoka,” amesema Mr Blue.
Kauli hiyo imefungua ukurasa mwingine katika historia ya muziki wa Mr Blue, hasa kuhusu namna baadhi ya nyimbo zake zilivyoibuka na changamoto alizokutana nazo katika hatua za mwanzo za safari yake ya muziki.




