Shakira arejea Madrid kwa maonesho 12

MADRID: MWANAMUZIKI wa kimataifa, Shakira Mebarak, kesho ataendelea na mfululizo wa maonesho yake mjini Madrid, Hispania, huku mashabiki wake wakisubiri kwa hamu kumuona tena nyota huyo akipanda jukwaani katika mfululizo wa maonesho 12 nchini humo.
Shakira, ambaye amekuwa kivutio katika ziara hiyo, anatarajiwa kuendelea kuwalisha burudani mashabiki wake kwa kuimba na kutumbuiza nyimbo zake zinazomfanya kuwa mmoja wa wasanii wanaofuatiliwa na mashabiki wa muziki duniani.
Baada ya maonesho ya kesho, Oktoba 2, Shakira ataendelea na maonesho mengine Oktoba 3 na 4, kabla ya kurejea tena jukwaani Oktoba 9, 10 na 11.
Ratiba hiyo inatarajiwa kufikia tamati Oktoba 11, huku mashabiki wa Madrid wakipewa nafasi zaidi ya kushuhudia moja kwa moja uwezo wa msanii huyo katika muziki na burudani.
Kurejea kwa Shakira nchini Hispania kumeongeza hamasa miongoni mwa mashabiki wake, hasa kutokana na muda uliopita tangu alipofanya maonesho makubwa nchini humo.
Shakira amekuwa na safari ndefu katika muziki wa kimataifa, akijenga jina kubwa kupitia nyimbo zake za lugha ya Kihispania na Kiingereza, huku akiendelea kuwa na mashabiki katika maeneo mbalimbali duniani.




