Rambo aliogopa kifo kutengeneza filamu ya maisha yake ‘I Play Rocky’

NEW YORK: MWIGIZAJI maarufu wa Hollywood, Sylvester Stallone, amesema awali alikuwa na mashaka kuhusu kutengenezwa kwa filamu inayosimulia historia ya utengenezaji wa filamu yake maarufu ya Rocky, akijiuliza kama ilikuwa mapema mno kusimulia historia ya maisha yake wakati bado yuko hai.
Stallone alitoa maoni hayo alipokuwa akizungumzia kitabu chake kipya cha kumbukumbu za maisha yake, ‘The Steps’, katika mazungumzo yaliyofanyika 92NY jijini New York, Marekani.
Filamu hiyo mpya, inayojulikana kwa jina la ‘I Play Rocky’, inaelezea safari ya utengenezaji wa filamu ya Rocky iliyotoka mwaka 1976, pamoja na changamoto alizokutana nazo katika kuhakikisha mradi huo unakamilika.
Akizungumzia mashaka yake ya awali kuhusu filamu hiyo, Stallone alisema alijiuliza kama watayarishaji walikuwa wanawahi kusimulia historia yake, akisisitiza kuwa bado hajafariki.
Hata hivyo, alisema mtazamo wake ulibadilika baada ya kuona uigizaji wa Anthony Ippolito, ambaye anacheza nafasi yake akiwa kijana katika filamu hiyo.
Rambo alieleza kuwa kuna baadhi ya picha na namna Ippolito alivyoigiza zilizomfanya ahisi kana kwamba anajitazama mwenyewe akiwa kijana, jambo lililomvutia kutokana na kufanana kwao katika baadhi ya mienendo.
Alifafanua kuwa hakuhusika moja kwa moja katika utayarishaji wa ‘I Play Rocky’, iliyoongozwa na Peter Farrelly, akisema aliamua kuiacha timu ya watayarishaji ifanye kazi yake yenyewe huku akiwa tayari kutoa majibu endapo angehitajika.
Katika mazungumzo hayo, Rambo pia alizungumzia kutoridhishwa kwake na filamu ya ‘Rocky V’ iliyotoka mwaka 1990, akisema anatamani kupata nafasi ya kuifanyia marekebisho upya kwa kushirikiana na kampuni ya Amazon.
Filamu ya awali ya Rocky, iliyotolewa mwaka 1976, ilimjengea Stallone umaarufu mkubwa duniani na kuwa sehemu muhimu ya historia ya filamu za michezo na mapambano ya maisha katika tasnia ya Hollywood.




