Ahmad Ally ataja chanzo cha kipigo Kenya

NAIROBI: KOCHA Mkuu wa Timu ya Taifa ya Tanzania ya U23, Ahmad Ally, amesema makosa ya kiulinzi na kutokuwa na mpangilio mzuri wakati timu haikuwa na mpira yamechangia kikosi chake kupoteza kwa mabao 4-1 dhidi ya Kenya katika mchezo wa kufuzu AFCON 2027, uliochezwa jana Uwanja wa Nyayo.
Ahmad amesema kipindi cha kwanza hakikuwa kibaya kwa upande wao, lakini mabao waliyofungwa yalitokana zaidi na kushindwa kudhibiti nyakati za mabadiliko ya mchezo, huku timu ikipoteza baadhi ya nyakati ambazo ilipaswa kuzitumia kupata faida.
Amesema kipindi cha pili pia walifanikiwa kuudhibiti mchezo kwa nyakati kadhaa na kupata nafasi ya kufunga, lakini kupoteza umakini kuliwapa Kenya nafasi ya kuongeza mabao.
“Hatukuwa vizuri kwenye organization, hasa off the ball. Mabao ya tatu na ya nne yanafanana, yametokana na makosa binafsi ambayo tumeyafanya. Tunahitaji kuwa bora zaidi kwenye mchezo unaofuata na kutumia vizuri nyakati zinazojitokeza,” amesema Ahmad.
Akizungumzia maendeleo ya soka la vijana nchini, Ahmad amesema anajivunia kuona wachezaji wengi wanaopata nafasi katika timu mbalimbali wakipitia mfumo wa timu za vijana, akitaja U17 na U20 kuwa sehemu muhimu katika mchakato huo.
Amesema hali hiyo inaonesha kuna maendeleo katika kuwaendeleza vijana kutoka kundi moja la umri kwenda jingine, ingawa bado kuna kazi ya kufanya ili kuwajenga zaidi na kuwapa muda wa kutosha wa kuendelea kuboresha uwezo wao.
“Ni jambo la kujivunia kuona kuna maendeleo kwa vijana katika kila kundi la umri na tunaona tunaweza kushindana. Tunahitaji kuendelea kupata muda zaidi wa kuboresha kila siku katika kila kundi ili kufikia malengo yetu,” amesema Ahmad.




