Muziki

Isha Mashauzi kuathimisha miaka 20 ya muziki wake Oktoba 24

DAR ES SALAAM: MSANII wa muziki wa taarab, Isha Mashauzi maarufu kama “Jike la Simba”, anatarajia kuadhimisha miaka 20 ya safari yake ya muziki katika tamasha litakalofanyika Oktoba 24, katika ukumbi wa Super Dome, Masaki jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Isha Mashauzi amesema alianza rasmi safari yake ya muziki mwaka 2006 na sasa anafikisha miaka 20 tangu aanze kufanya muziki.

Amesema katika safari hiyo amepitia hatua mbalimbali huku akipata msaada na ushauri kutoka kwa watu mbalimbali, wakiwemo watangazaji ambao wamekuwa wakitoa nafasi kwa kazi zake na kumshauri katika safari yake ya kimuziki.

Akizungumzia mchango wa watangazaji katika mafanikio yake, Isha amesema Gea Habibu anawakilisha kundi la watangazaji waliomuunga mkono kwa miaka yote ya safari yake ya muziki.

Kwa upande wake, msanii mkongwe wa taarab Khadija Kopa, ambaye ameeleza kuwa anamchukulia Isha Mashauzi kama mtoto wake, amesema amemfahamu tangu akiwa mdogo na alitambua mapema uwezo wake wa kuimba.

“Kama mama wa Isha Mashauzi, namjua. Anachofanya anakifanya vizuri.

Nililetewa akiwa mdogo, alikuwa anaimba na alikuwa akivizia nikienda jikoni, anachukua nguo zangu kabatini na kwenda kuimba.

Ana uwezo mkubwa, anaweza kumiliki jukwaa na anajua muziki na anachokifanya,” amesema Khadija Kopa.

Katika tukio hilo, Afisa Sanaa Mwandamizi wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Abel Ndaga, amewakaribisha wasanii na wadau mbalimbali wa sanaa kufika BASATA kwa ajili ya kupata ushauri na huduma zinazohusiana na shughuli zao za kisanaa.

Ndaga amesema BASATA iko tayari kutoa ushirikiano kwa wasanii wanaohitaji msaada au ufafanuzi kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu sanaa.

Naye Juma Mbizo, ambaye ni baba mlezi wa Isha Mashauzi, amesema yeye ni miongoni mwa watu waliomshika mkono msanii huyo katika hatua mbalimbali za safari yake ya muziki hadi kufikia mafanikio aliyonayo leo.

Maadhimisho hayo ya miaka 20 yanatarajiwa kuwa sehemu ya kumuenzi Isha Mashauzi kwa safari yake ndefu katika muziki pamoja na kuwashirikisha mashabiki, wasanii na wadau mbalimbali waliokuwa sehemu ya safari yake.

Related Articles

Back to top button