Muziki

Nandy: Narudi jukwaani kwa staili nyingine

DAR ES SALAAM:MSANII wa muziki Faustina Charles ‘Nandy’ amesema amepokea maelekezo ya Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kuhusu mavazi na yuko tayari kuyazingatia katika tamasha lake linalotarajiwa kufanyika kesho jijini Dar es Salaam, akisema lengo lake ni kuhakikisha mashabiki wanapata burudani.

Nandy amesema anaheshimu maelekezo ya BASATA na anakubali pale anapokosea, akieleza kuwa yeye na timu yake wamekuwa wakijifunza kutokana na changamoto zinazojitokeza katika safari yake ya muziki.

Amesema hata hivyo, suala la mtu kuvutiwa au kutamani kutokana na vazi ni jambo ambalo si rahisi kulidhibiti kwa sababu kila mtu ana namna yake ya kutafsiri anachokiona.

“Tunapokosea tunakubali, na nashukuru wameona hilo. Kesho tunafanya shoo, tutazingatia maelekezo tuliyopewa na tunataka watu waje kuburudika,” amesema Nandy, huku akisisitiza kuwa maandalizi ya tamasha hilo yanaendelea vizuri.

Amesema katika tamasha hilo mashabiki watarajie muziki, dansi na ubunifu wa aina mbalimbali, huku akiahidi kupanda jukwaani akiwa na uhuru wa kufanya kazi yake bila kuvunja taratibu.

Kwa upande wake, Meneja wa Nandy, John Mchaina, amesema waliamua kwenda BASATA ili kupata mwongozo kuhusu mavazi ambayo msanii huyo atatumia kwenye tamasha hilo, wakiamini kuwa ni muhimu kujua mapema kama yanakidhi kanuni na maadili ya sanaa. Amesema walifikisha suala hilo kwa BASATA ili kupata maelekezo kabla ya shoo.

Mchaina amesema walipozungumza na BASATA walipewa maelekezo kuhusu namna Nandy anavyopaswa kuvaa, ikiwemo kuepuka mavazi ambayo yanaweza kutafsiriwa kuwa hayana staha.

Amesema wao wanaamini sanaa inapaswa kuendelea kukua na kufikia viwango vya kimataifa, akitolea mfano namna ubunifu wa Nandy katika mavazi ulivyoendelea kuzungumzwa katika nchi mbalimbali za Afrika.

Related Articles

Back to top button