Nyumbani

Wasanii kusubiri mgao wa Sh bilioni mbili Novemba

DAR ES SALAAM: WASANII nchini wanatarajiwa kunufaika na mgao wa Sh bilioni mbili zilizokusanywa kupitia mfumo wa hakimiliki, huku Serikali ikipanga kufanya tukio maalumu la kugawa fedha hizo Novemba mwaka huu.

Akizungumza kuhusu suala hilo Leo Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Paul Makonda amesema fedha hizo zitatolewa kwa wasanii kama sehemu ya mapato yanayotokana na kazi zao, tukio la ugawaji likitarajiwa kuhudhuriwa na kiongozi mkubwa.

Amesema maandalizi ya tukio hilo yanaendelea, akisisitiza kuwa lengo ni kuhakikisha wasanii wanapata manufaa kutokana na kazi wanazozalisha na haki zao za ubunifu.

“Sh bilioni mbili imekusanywa na itatolewa kama gawio,” amesema. Kwa mujibu wa Waziri, tukio hilo linatarajiwa kuwa sehemu ya hatua za serikali kuimarisha mfumo wa hakimiliki na kuhakikisha fedha zinazokusanywa zinawafikia wahusika kwa utaratibu unaotambulika.

Aidha, Serikali inaendelea kupitia mfumo wa ukusanyaji wa mapato ya hakimiliki kutokana na mabadiliko yaliyotokea katika matumizi na usambazaji wa kazi za wasanii.

Waziri amesema mfumo huo uliandaliwa wakati ambapo matumizi ya kazi za wasanii yalitegemea zaidi bidhaa kama CD, lakini maendeleo ya teknolojia yamebadili kwa kiasi kikubwa namna muziki, filamu na maudhui mengine yanavyotumiwa.

Kutokana na hali hiyo, Serikali inaangalia vyanzo vipya vya mapato vitakavyoweza kuendana na mazingira ya sasa ya kidijitali na kuwawezesha wasanii kunufaika zaidi na kazi zao.

Related Articles

Back to top button