Clara atinga Ubalozi wa Marekani

DAR ES SALAAM: UBALOZI wa Marekani nchini Tanzania umempongeza, ukimtakia kila la heri nyota mpya wa Washington Spirit ya Marekani, Mtanzania, Clara Luvanga.
Clara alipata pongezi hizo alipokuwa ofisi za ubalozi huo leo Jumatano baada ya kupokea mwaliko na kuzungumza naye juu ya safari yake ya soka, waliyoiita yenye kutia moyo.

Taarifa iliyowekwa mtandaoni na ubalozi huo imeeleza kuvutiwa na nyota huyo, 21 kuwa mchezaji wa kwanza kutoka Tanzania kushiriki ligi ya NWSL tangu kuanzishwa kwake.
“Tulipata fursa ya kumkaribisha Clara katika Ubalozi wa Marekani, ambako alikutana na timu yetu ya Diplomasia ya Umma na kutushirikisha safari yake ya soka yenye kutia moyo.
“Wakati Marekani ikiadhimisha Muongo wa Michezo, ikiwemo Kombe la Dunia la FIFA 2026 na Michezo ya Olimpiki na Paralimpiki ya Los Angeles 2028, safari ya Clara inaonesha jinsi michezo inavyounganisha nchi zetu na kuhamasisha kizazi kijacho.
“Hongera sana, Clara! Tunakutakia kila la heri katika mechi yako ya kwanza jijini Washington mwishoni mwa wiki hii,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Mshambuliaji huyo wa zamani wa Dux Logrono ya Uhispania, alijiunga na Washington akitokea Al-Nassr ya Saudi Arabia baada ya misimu mitatu ya mafanikio.
Staa huyo ambaye sasa ndiye mchezaji ghali zaidi kwa wanawake duniani, akitua Marekani kwa kitita cha Dola milioni 2.3, anatarajiwa kuwa uwanjani Septemba 27, mwaka huu dhidi ya Angel City FC.




