Zuchu, Diamond waadhimisha Henna Day kuelekea siku 40 za mtoto wao

DAR ES SALAAM: SHAMRASHAMRA za kuelekea kuadhimisha siku 40 tangu kuzaliwa kwa mtoto wa mastaa wa muziki nchini, Zuchu na Diamond Platnumz, zimeendelea baada ya kufanyika kwa hafla maalum ya Henna Day nyumbani kwa mama Diamond.

Katika hafla hiyo iliyopambwa kwa mandhari ya kuvutia na kuakisi tamaduni za Pwani, Zuchu alikuwa miongoni mwa wahusika wakuu wa tukio hilo, ambapo alionekana akiwa amevalia mavazi mbalimbali, yakiwemo mavazi ya sare ya kijora yaliyovaliwa pia na baadhi ya wageni.
Mbali na kupendeza kwa mavazi, Zuchu alionekana akiwakaribisha wageni, akiimba na kufurahia muziki pamoja na washiriki wengine wa hafla hiyo.

Katika baadhi ya matukio, Zuchu pia alionekana akila chakula pamoja na Diamond Platnumz, ambaye alikuwa amevalia vazi jeusi, huku wawili hao wakionekana kufurahia muda wao katika shamrashamra hizo.
Mandhari ya hafla hiyo yalipambwa kwa ustadi, ambapo rangi nyekundu ilitawala pamoja na mavazi yenye mitindo ya mahadhi ya mwambao wa Pwani na tamaduni za Kiislamu.

Wageni mbalimbali, wakiwemo mastaa kama Nandy, Billnass, Jux, Fayvann na wengine wengi, walijitokeza kushiriki hafla hiyo, huku baadhi yao wakichorwa henna, mapambo yanayopendwa na wanawake na yenye nafasi muhimu katika baadhi ya desturi na tamaduni.
Hafla hiyo ni sehemu ya shamrashamra zinazoendelea kuelekea kilele cha maadhimisho ya siku 40 tangu kuzaliwa kwa mtoto wa Zuchu na Diamond Platnumz, tukio ambalo limeendelea kuvuta hisia za mashabiki wa mastaa hao.




