Fatma: Mashabiki wasituchoke, tumejifunza

KIGALI: MCHEZAJI wa Simba Queens, Fatma Issa, amewaomba mashabiki wa timu hiyo kuendelea kuwaunga mkono licha ya kutolewa kwenye mashindano ya kuwania kufuzu Ligi ya Mabingwa Afrika kwa Wanawake (CAF Women’s Champions League) kupitia michuano ya CECAFA.
Simba Queens ilishindwa kuvuka hatua ya makundi baada ya kupata matokeo yaliyowafanya kuaga mashindano hayo, huku Kenya Police ikifanikiwa kusonga mbele.
Fatma amesema matokeo hayo yamewaumiza wachezaji wote, lakini wameyachukulia kama funzo muhimu katika kujiandaa na mashindano mengine yanayokuja.
“Kwa ukubwa wa timu yetu, kiukweli tumefanya vibaya na hakuna mtu aliyefurahia haya matokeo. Nina imani kila mchezaji ameumia, lakini tumeyachukulia kama funzo la kujipanga kwa mashindano mengine yanayokuja mbele yetu,” amesema Fatma.
Amesema mchezo wa soka una matokeo matatu na kilichowakuta Simba Queens ni sehemu ya ushindani, huku akisisitiza kuwa makosa waliyofanya yalitumiwa na wapinzani wao.
Fatma ameongeza kuwa wachezaji wanaona uzito wa matokeo hayo kwa kuwa wamewakilisha Simba Queens pamoja na Tanzania, lakini wameamua kuyageuza kuwa somo la kuboresha kiwango chao katika mashindano yajayo.
Simba Queens sasa italazimika kurejea na kujipanga upya kwa ajili ya mashindano mengine, huku lengo likiwa kuboresha kiwango na kurejea kwa nguvu katika michuano ya kimataifa.




